Neno la Siku 9: Kumbukumbu 6:4–5

Kumbukumbu 6:4–5

Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.

Baada ya kutoka Misri, kupewa sheria na kufanya agano na Mungu, kujenga hema kwa ajili ya kukutana na Mungu, kuzunguka-zunguka jangwani miaka 40, wakitolewa na Bwana Mungu chakula na maji, Waisraeli walikaribia kuingia nchi iliyahidiwa na Mungu kwa Ibrahimu. Na hapo Musa alisema nao. Musa mwenyewe hataingia nchini, atafariki. Bali katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, tunasoma mahubiri yake ya mwisho kwa taifa la Israeli.

Hapa anawaelekeza kwa moyo wa Agano. Anawaambia mambo mawili: Mungu ni Mmoja na Mpende.

Bwana Mungu aliyewaokoa kutoka Misri ni Mmoja. Ni tofauti na miungu walioabudiwa na mataifa mengine, wakiwa wengi, au wakiwa na sanamu au sura nyingi. Ni mmoja. Lakini, kwa kuwaokoa toka Misri, akishinda sanamu zao na vile walivyoita miungu, Bwana Mungu alithibitisha kuwa yeye ni Mungu na hakuna mwingine (unaweza kusoma wazo hili katika Kumbukumbu 4:31–36, na pia 4:39). Bwana ni Mungu na hakuna mwingine.

Hivyo Wampende. Kumpenda Mungu ni sharti la Agano lao walilolifanya naye, bali pia ni tokeo wazo la kwamba ni Mungu na hakuna mwingine. Wampende! Kumpenda Mungu ni kutii amri zake, kuzishika kwa juhudi, kwa uelewa, kwa uchaji. Hapa Waisraeli wanaambiwa kumpenda Mungu kwa moyo wote, roho yote a nguvu zote. Moyo kwa lugha nyingine ni nia au mapenzi. Roho kwa lugha nyingine ni hisia na mawazo. Nguvu kwa lugha nyingine ni matendo. Hivyo, hawana budi kumpenda Mungu kwa matendo yao yote, mawazo na hisia vyao vyote, na nia au mapenzi yao yote. Watatimiza hivi hasa kwa kufuata maagizo aliyowapa.

Yesu mwenyewe alisema amri hii ni amri kuu, na kwamba katika amri hii na ya pili ya kumpenda jirani ‘hutegemea torati yote na manabii’ (Mathayo 22:36–40). Hivyo wafuasi wa Yesu nao pia wanaitwa wampende Mungu kwa moyo wote, roho yote, nguvu zote. Wafanye hivi kwa sababu Mungu ni Mmoja na aliwaokoa kutoka ufalme wa giza kama alivyowaokoa Waisraeli toka Misri. Lakini pia, Yesu huonyesha jinsi ya kutii amri hiyo, alipoenda msalabani kufa. Alifanya hivyo kwa ajili ya kutii Mungu Baba yake, kumpenda Baba kwa moyo wake wote, na roho yake yote, na nguvu zake zote (unaweza kusoma wazo hili katika Yohana 14:30–31). Kwa hiyo, Yesu anatimiza amri hiyo msalabani, na kutupa mfano wa namna ya kumpenda Mungu.

Inatupa changamoto mbili. Kwanza, tushukuru kuwa sheria imetimilizwa katika Yesu na kifo chake. Hatumkaribii Mungu kwa Agano lile la Kale, bali kwa Agano Jipya ambalo Yesu alifanya kwa damu yake. Tunamkaribia Mungu katika Yesu, kwa neema, na kwa imani. Hivyo, wokovu si jambo la kutii sheria, bali ni kumwamini Yesu — alitii sheria kwa niaba yako ili upate kusamehewa. Tushukuru, lakini pia, tuache kutegemea matendo yetu, na tushike Yesu kwa imani ili atuokoe.

Pili, tumfuate Yesu kwa upendo huo. Alituonyesha namna ya kumpenda Mungu — alijitoa nafsi yake katika utii kwa Baba. Sisi nasi, kwa Roho Mtakatifu, tujitahidi kumpende Mungu jinsi hii hii, tujikane na kujitoa nafsi zetu kwa ajili yake katika utii na upendo wote. Upendo huo utakuwa wa moyo wote, roho yote na nguvu zote, na utafaa kabisa, tukikumbuka tu, unatokana na wokovu. Katika waraka kwa Warumi inasema hivi:

12:1 Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.

Bwana Yesu atusaidie!

Neno la Siku 8: Marko 10:45

Marko 10:45 — Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Kwa maneno hayo Yesu aliwakemea na kufundisha wanafunzi wake. Wanafunzi walitafuta nafasi ya juu. Hata Yohana na Yakobo waliomba vyeo vya juu sana wakati Yesu atakapoingia ufalme wake (Marko 10:37). Na Yesu akajibu kwa kusema utawala au uongozi kwa ufalme wake ni tofauti sana na ule wa dunia. Kwa kuwa Mungu anampa mtu mamlaka ili awatumikie wengine. Ni tabia yake Mungu. Tabia hiyo inafunuliwa wakati Mungu Mwana alijitwaa utu wetu akishuka ulimwenguni kuwaokoa wanadamu waliokuwa wenye dhambi na maadui (Fil 2:6–9).

Hapa Yesu anasema utawala au mamlaka yake inaonekana katika kujitoa nafsi yake kwa wengi. Anamaanisha wakati wa kusulubiwa msalabani. Alikufa si kwa dhambi zake kwani hana dhambi. Alikufa kwa ajili ya dhambi wa wanadamu ili awaokoe kwa kufa badala yao. Kama mwana-kondoo alivyokufa badala ya mtoto wa kwanza wakati wa Pasaka (Kutoka 12), vivyo hivyo Yesu alikufa badala ya wenye dhambi ili wapatanishwe na Mungu. Ndio wokovu wetu — kwa neema ya Mungu ametutolea mbadala, mwana wake mwenyewe, ili tusihukumiwe bali tupokee uzima wa milele. Hatukustahili zawadi hiyo, bali mfalme wetu na mfalme wa ulimwenguni alitumia mamlaka yake yote kwa ajili ya kujitoa uhai wake ili sisi wadogo na viumbe vyake tupate kuishi.

Na Yesu anasema ndivyo ilivyo mamlaka kwa mtazamo wa kikristo. Ni jinsi alivyotawala yeye — kutumika na kujitoa nafsi yake. Na ni jinsi wafuasi wake wanavyopaswa kutawala. Katika familia zetu, makanisa yetu na jamii zetu hakuna nafasi kwa mfuasi wa Yesu kutumia mamlaka yake kwa ajili ya mambo ya ubinafsi, au kujipenda, au kutawala kwa nguvu au udhalimu. Mamlaka tuliyopewa na Mungu si kwa faida yetu bali ni ili tupate kuwapenda wengine jinsi Mungu alivyowapenda. Si sababu kuacha kuongoza au kuacha kuamua au kuacha wajibu na mamlaka. Hapana. Ni kutumia mamlaka kwa ajili ya wengine na sio mimi.

Ikiwa mchungaji au Baba au mtumishi au mwalimu au mzee au mkuu anafuata Yesu hakuna nafasi kwa ubinafsi katika uongozi wake. Amepewa mamlaka na Munug kwa ajili ya wengine. Ajitahidi kumwiga Yesu. Aache kutumikiwa bali atumike. Ajitoe nafsi yake kwa wengine. Ndio sababu hapa Munguishi kusudi letu  ni kufundisha viongozi wa kutumikia. Ndiposa watamfuata Yesu.

Bwana Yesu atusaidie!

Neno la Siku 7: Mwanzo 22:1–2 (Sehemu B)

Mwanz0 22:2 — Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.

Mwanzo 22:14 —  Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana.

Tumeshaangalia imani ya Ibrahamu katika kifungu hiki (Soma hapa). Kifungu hiki lakini, kinahusu Mungu hasa. Ni Mungu anayeanzisha tukio (m. 1–2) na mwishoni ni Mungu anayesifiwa kwa kumtolea Ibrahimu. Kifungu kinahitimisha na tukio la Ibrahimu kupaita mahali pale ‘Mungu atatoa’ au kwa kiebrania, ‘Yehova-yire’ (Yahwe-yire).

Imani ya Ibrahimu ni katika Mungu atoaye. Alipoulizwa na mwanawe kondoo ya kuchinja yuko wapi, Ibrahimu alijibu, ‘Mungu atatoa’ (m. 8). Baada ya kuzuiliwa na malaika ya Bwana na kukuta kondoo dume aliyetolewa, Ibrahimu alipaita pale ‘Mungu atatoa’. Mungu atatoa.

Bali, labda unajiuliza, Mungu aliwezaje kumwambia Ibrahimu kumchinja mwanawe? Kuna sababu tatu kuu. Kwanza ni kuonyesha mfano wa neema yake katika kutuma Yesu Kristo mwanawe afe kwa ajili ya ulimwengu. Pili ni kuonyesha gharama kuu ya dhambi. Uasi wa binadamu unatakiwa mauti. Sadaka  ya kutekesa ni ile sadaka ya dhambi. Baadaye atawaruhusu Waisraeli kutoa wanyama, bali wanyama ni mfano tu na hawawazi kuondoa dhambi (taz. Ebr 10:4). Sababu ya tatu ni kuonyesha ubatili na uovu wa dini zingine za watu waliozunguka Ibrahimu.

Kwa kumwambia Ibrahimu kuchinja mtoto wake Mungu hakupinga mapenzi yake wala sheria zake za AK. Alifanya hivi kuonyesha Ibrahimu tatizo na uovu la dini nyingine ambazo majirani yake walizifuata. Dini nyingine ni za binadamu na hata leo zinataka sadaka kubwa sana ya watu. Kutoa nafaka mwaka huu unaleta mavuno makubwa, lakini mwaka ufuatao mavuno ni madogo, hivyo wanatoa nafaka na mnyama. Halafu inaongezeka tena na tena, mpaka watu wanatoa uhai wa watoto wao wa kwanza. Angalia, kwa mfano, Mika 6:6-8.

Mungu ni tofauti lakini. Mungu ni yule atoaye. Kwa hiyo, alizuia Ibrahimu kutoa mwanawe ili apate kuonyesha neema yake katika kutoa mwenyewe. Ni kama alisema na Ibrahimu — tufanye kama dini nyingine kuangalia jinsi zilivyo. Halafu anampeleka kiini kabisa ya dini hizi za binadamu kumwonyesha ubaya wao. Halafu akasema, inatosha. Acha. Angalia nimekutolea.

Mungu ni tofauti kabisa. Hachukue anatoa. Hapendezwi na majaribu ya wanadamu kumpendeza kwa sadaka zao, bali anapendezwa kuwatolea kwa wingi wa rehema yake. Badala ya kudai anawapa watu bure na kwa neema.

Ndio maana kuu ya kifungu hiki: Mungu atatoa. Na kwa kweli kifungu ni kivuli cha tukio kuu la Biblia, wakati Mungu alitoa mwana wake kuwa sadaka kwa ajili ya dhambi za wanadamu. Historia hii ni picha ya kazi ya Mungu aliyoitenda katika kutoa mwana wake mpendwa kufa na kupokea ghadhabu yake badala yetu.

Mungu atatoa.

Alitoa kondoo badala ya Isaka. Alitoa mwana wake afe badala yetu. Hivyo hatutakiwi kufa tena ikiwa tumtegemee Yesu tu.

Mungu atatoa.

Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? (Rum 8:31–32).

Bwana Asifiwe!

Neno la Siku 6: Mwa 22:1–2 (sehemu A)

Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.

Bila shaka neno hili ni gumu. Mungu alimjaribu Ibrahimu kwa kumwambia amchinje mwanawe. Ni kama Mungu alinyoosha imani ya Ibrahimu kama kuvuta sana kamba mpaka kiasi cha kuharibika, na dakika za mwisho akatuma malaika kumrehemu Ibrahimu asimchinje mwanawe. Na tunaambiwa Ibrahimu alitenda kwa imani safi na kwa hivyo Mungu alipendezwa naye.

Ilikuwa nini juu ya imani ya Ibrahimu ambayo ilimpendeza Mungu?

Imani yake ililingana na neno ambalo Mungu alilosema. Mungu alikwishamwahidi Ibrahimu kwamba watoto wake na tena Isaka atarithi nchi na kuwa taifa kuu. Fikiria alichosema hata katika 21:12 — “katika Isaka uzao wako utaitwa” (Taz. pia 12:7; 15:4, 18; 17:19, 21). Ibrahimu aliahidiwa na Mungu juu ya Isaka kwamba Mungu atabariki ulimwengu kupitia Isaka na watoto wake. Hivyo, alipoenda kumchinja Isaka imani yake haikuwa tumaini bure tu, bali ilikuwa imani katika neno la Mungu. Bila shaka hakuelewa kwa jinsi gani inavyowezakutokea, bali alitegemea Mungu na ahadi zake kumfanya Isaka kuwa taifa kuu. Kwa hivyo alitii neno la Mungu kumchinja akiamini kwa jinsi fulani Mungu atatimiza ahadi yake.

Tutulie hapa. Hii ni muhimu sana kupata. Imani halisi ni kuamini neno la Mungu na kukubali ahadi zake. Watu wengi wanaweza kuwa na matumaini na kusema naamini jambo fulani. Lakini si imani halisi. Kwa mfano, naweza kusema naamini Mungu ataniponya, au kunibariki na watoto, au kunisaidia katika mitihani yangu. Lakini tofauti na Ibrahimu sina neno wala ahadi ya Mungu juu ya vitu hivi.

Imani halisi inazalishwa na neno la Mungu na ni kulingana nalo. Mfano mwingine. Naamini mke wangu ananipenda kwa sababu aliniambia. Nina neno na nategemea neno hili kuwa kweli. Bali sina neno la mtu mwingine, kwa mfano, Malkia Elizabeta kwamba ananipenda, kwa hiyo nitakuwa kichaa kusema, naamini naye Malkia ananipenda.

Imani inatokana na Ahadi au Neno. Hivyo, Ibrahimu alienda kumchinja kwa kutegemea neno la Mungu lililosema ‘katika Isaka’ nitakufanya taifa kuu. Hakujua jinsi Mungu atakavyofanikisha bali alitegemea neno lake ni kweli. Hatuwezi kutegemea Mungu atafanya jambo ambalo hakusema atalifanya. Bali yote aliyoyasema atafanya hakika atafanya, hata ikiwa hatujui kwa vipi aweza kufanya, na kwa hiyo inatubidi kutegemea yote aliyoyasema na kuamini.

Ndivyo namna Mwandishi wa Waebrania alivyotafisi imani ya Ibrahimu. Alisema kwamba, Ibrahimu, baada ya kupokea ahadi na amri hii ya Mungu akatafakari, halafu ‘akahesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu’ (Ebr 11:19). Au kama Mungu alivyowahi kusema na Ibrahimu, alipoahidi kuzaliwa kwa Isaka, ‘Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?’ (Mwa 18:14). Paulo alifafanua neno hili kwa kusema Ibrahimu ‘akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.’ (Rum 4:21)

Ibrahimu anatufundisha juu ya imani. Imani haiwezi kushindwa na mazingira na matukio bali inashika neno na ahadi za Mungu kwa kujua hakika Mungu atatimiza — kwa njia yake na wakati wake, ndio, bali atatimiza. Bali muhimu sana tukumbukea kwamba imani inazalishwa na neno la Mungu na si vinginevyo.  Kwa hiyo, lazima imani iongozwe kwa neno. Na imani inalishwa au kuongezwa kwa kusikia tena na tena neno la Mungu. Tunaambiwa pengine, ‘imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo’. (Rum 10:17).

Tujitahidi kusoma na kusikia neno la Mungu kila siku na kupokea kwa imani. Tena, tujitahidi kuamini vile Mungu alivyosema tu na si zaidi wala si maneno yasiyo ya Mungu.

Bali kifungu hiki kinafundisha mambo mengine tena, na ni muhimu hata kuliko imani ya Ibrahimu. Kifungu hasa ni picha ya msalaba na pia inaonyesha ukarimu na wema wa Mungu. Tutasema juu ya mambo hayo siku nyingine. Karibu!

Neno la Siku 5: Tit 3:14

Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.

Mstari huo una maana wa kina, ila tunaweza kupita tu bila kuielewa. Kwanza tunaona kuwa wafuasi wa Kristo hawana budi kufanya na kuzidi katika matendo mema, au matunda. Haya si kwa ajili ya wokovu, kama alivyowahi kusema, Mungu alituokoa si kwa sababu ya matendo mema yetu (3:5), bali yatoka au kuzalishwa kwa wokovu. Tena ni neema tu, kwa sababu ni Neema inayofundisha kukataa ubaya na kumwishia Yesu (2:11-14). Kwa hiyo, kama tunavyofahamu, tuenende katika matendo mema (taz. pia 2:14, 3:8).

Bali jambo la kushangaza hapa ni neno lile kujifunza: ‘watu wetu nao wajifunze’. Yaani, kutenda mema si jambo ambalo tunafahamu tangu awali au ni asili yetu. Tunapookoka, tunapaswa kuanza kujifunza njia zake Yesu ili tupate kuenenda kwao. Tunahitaji kujifunza au kufundishwa kufanya mema. Ndiyo sababu Paulo aliwahi kusema ‘kunena’ au kufundisha mambo hayo (2:14). Ndiyo sababu Yesu alipotuma wanafunzi kufanya wanafunzi alisema wawafundishe kutii kila alichowamuru. Yaani, sehemu ya kuwa mwanafunzi wa Yesu ni kujifunza au kufundishwa namna ya kuishi na jinsi ya kufanya mema.

Si kwa asili au desturi bali kwa neno la Mungu ambayo tunajifunza kufanya mema. Hivyo tujipe sharti kusoma na kujifunza, kutafakari na kutumia neno la Mungu kwa uchaji na kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu ili tuweze kufanya mema kweli kweli. Na Mungu atusaidie!

Neno la Siku 4: Mwa 6:5

Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote

Kwa mstari huu tunasoma kipimo au hukumu ya Mungu juu ya wale wanadamu aliowaumba kuwa mfano wake. Badala ya kuakisi wema na utakatifu wake ulimenguni, hawa wanadamu walimwasi na kujaza duniani na maovu. Mwanzo 3-11 inaeleza namna dhambi na kifo vilivyoenea duniani — na hapa ndicho kilele cha kwanza, na cha pili ni mnara wa Babeli ambapo watu walijaribu kumwondoa Mungu kabisa.

Mstari huu unaeleza sababu ya Mungu kutuma gharika na kusafisha uumbaji wake na wale walioujaza na uovu wao. Ni changamoto kwetu kwa sababu inatuonyesha kwamba wana wa Adamu si watu wema walio na mabaya machache, bali tuliathiriwa na dhambi kwa kila namna. Sikiliza lugha yake: kwanza— maovu ni ‘makubwa duniani’ — yaani ni mengi na ni kila mahali. Pili, si makusudi chache ya moyo, bali ni ‘kila kusudi’, na tatu, si mara kwa mara, bali ni ‘siku zote’. Yaani, kwa mahali ni pote. Kwa watu ni wote. Kwa muda ni siku zote. Kila mtu, kila kusudi, kila wakati na mahali — ni baya tu (hakuna mwema).

Ndio sababu tunaambiwa m. 6 kwamba: ‘Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.’ Ni kwa Biblia hukumu iliyo haki kwa dhambi ni mauti (Rum 6:23). Hivyo gharika.

Tunaambiwa gharika haikuweza kutatua shida hii ya dhambi kabisa, kwa sababu kwanza Nuhu alianguka halafu tukio lile la Babeli lilitokea. Na kupita Agano la Kale tunaambiwa mara baada ya mara juu ya dhambi na uasi wa wanadamu. Tunahitaji si gharika bali mwokozi anayeweza kutatua shida ya dhambi, na ndiye Yesu Kristo aliyeshinda dhambi kabisa kwa kufa kwake. Alipokufa alichukua dhambi zetu msalabani ili tusamehewe na ili tutakapofufuliwa naye tutaishi bila dhambi kabisa katika uumbaji mpya. Hata siku hizi, ingawa uwepo wa dhambi bado upo, tumewekwa huru na utawala wake ili tuongozwe na Roho.

Mtazamo wa Biblia ni tatizo la dhambi ni kubwa mno kuliko uelewa wetu, lakini pia suluhisho la Mungu kwa dhambi ni mzuri mno. Kwa lugha nyingine, mimi ni mwenye dhambi mkubwa, bali Yesu ni Mwokozi mkuu anayeweza kabisa. ‘Yeye [Yesu] asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye’ (2 Kor 5:21, taz. pia 1 Tim 1:15-17).

Bwana Yesu asifiwe!

 

Neno la Siku 3: Fil 3:9

nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani;

Hapa Paulo anaeleza haki aliyo nayo na ili aliyotafuta ni haki kutokana na Mungu. Zamani alijitahidi kupata haki yake mwenyewe katika kufuata sheria, bali alipomwona Kristo aliacha juhudi hizi zote akizihesabu kuwa mavi.

Badala ya haki kutoka kwa ndani alipewa kwa neema haki ya Kristo kutoka kwa nje. Kwa lugha nyingine tunaweza kusema ni haki ya kigeni. Kwa hiyo, kwa imani Paulo (na sisi pia kwa imani ile ile) anahesabiwa haki — na haki ambayo Mungu akaona si ya kwake, bali ni ya Yesu, na Paulo alivikwa nayo tu.

Jambo hili ni muhimu sana tunapofikiri kuhusu dhambi na wakristo. Ikiwa tunategemea haki yetu ya ndani, tunapofanya dhambi ni shida, tunaweza kuogopa usalama wetu tukiwa ndani  ya ufalme au la. Lakini, kwa sababu, Mungu anatuokoa kwa neema, akitufunika na haki ya Kristo na siyo yetu, hata tunapomkosea Mungu hamna shida — bado tunafichwa au kufunikwa na haki yake Kristo. Na haki hiyo ni kamilifu.

Kwa hivyo, kama Martin Luther alisema, mwamini ni mwenye haki na mwenye dhambi wakati mmoja. Ni mwenye dhambi kiasili, juu yake mwenyewe. Bali kwa neema na imani amevikwa na haki ya Kristo, na kwa hivyo wakati huo huo pia ni mwenye haki kabisa. Na Mungu anamhesabu haki.

Bwana Yesu Asifiwe!

Theolojia ya Kibiblia

Alama ya pili ya kanisa lenye afya ni Theolojia ya Kibiblia. Maana yake ni kuwa na mafundisho yenye uzima katika kanisa (2 Tim 1:3, Tito 1:9, 2:1). Biblia inafundisha mambo mengi na inatupasa kama wakristo kufahamu mafundisho hayo vizuri — kwa jinsi tunavyoweza.

Kwa kweli tuna mambo ya mapokeo yanayoweza kutusaidia, kama sharti 39, hotuba za Cranmer, na kitabu cha sala. Pia kuna imani ya mitume, ya nikea na ya athanasio. Bali chanzo pekee cha mafundisho yenye uzima ni Biblia — hatuna budi kusikia neno la Mungu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwa imani na utii.

Wanafunzi wa MBC wanatakiwa kusoma kwa kina zaidi mambo ya theolojia kwa sababu namna tunavyoelewa mafundisho ya Biblia kwa ujumla inatuathiri namna tunavyosoma kila sehemu na kuihubiri. Ni muhimu sana kupata kumfahamu Mungu kweli katika neno lake jinsi alivyojifunua na jinsi alivyotuambia juu ya binadamu na wokovu.

Umuhimu wa mtumishi si tu kuweza kunukuu andiko, bali kujua na kutumia kwa namna ambavyo inavyofanana na vingine (Mat 4:7). Ufahamu wa Mungu ulio halisi ni hekima iliyotoka juu (Yak 3:17) na pamoja na kufahamu mtu, italeta matendo mema katika maisha ya mtu.

Theolojia ni kama miwani tunayotumia kutazama ulimwengu kiukweli. Lakini, kiasili tumejifanya vipofu na tunadanganywa tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi (Tito 3:3). Kwa hivyo, bila theolojia ya kibiblia hatuwezi kuona kweli — lakini, kwa neema, Mungu anatupa ufahamu huo, kwa Roho Mtakatifu na neno lake, ili tuwe na nia ya Kristo (1 Kor 2:6-16). Bwana Yesu asifiwe!

Neno la Siku 2: 2 Kor 12:9-10

Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.  Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

Paulo aliandika maneno hayo baada ya kueleza mateso mengi yaliyompata katika maisha yake ya kumtumikia Kristo. Alieleza mambo mengi hayo kuonyesha alama halisi ya mtumishi wa Kristo ni kupokea mateso na kuyavumulia. Hivi ni sawa na Yesu mwenyewe (2 Kor 1:5-7). Lakini baada ya kuorodhesha mateso hayo, alitoa mfano wa kupata mwiba katika mwili. Hatujui mwibu huu ni nini na haiwezi kutufaa kudhani. Umuhimu ni kwamba upo na Paulo alijua na taabu kwa ajili  yake. Aliomba Mungu kuondoa, na Mungu alijibu namna hii tunayoona juu — ‘neema yangu yakutosha’.

Kuna mambo matatu kujifunza hapa. Kwanza, Paulo ingawa ni mtumishi mwema hakupokea jibu la ‘ndio’ alipoomba. Mungu alimfanyia wema kwa kusema ‘hapana’. Yaani ni bora aliendelee na mwiba huu, na kwa hiyo alipoomba uondolewe Mungu hakufanya. Mara nyingi tunafikiri watakatifu au wakubwa watapewa kila wanachokiomba. Hapa, lakini, twaona Mungu anafanya kwa kadiri ya mapenzi yake na kwa ajili ya wema wetu (taz. Rum 8:28).

Pili, Mungu anatumia udhaifu wa watumishi wake kuonyesha nguvu zake. Alisema, ‘uweza wangu hutimilika katika udhaifu’. Kwa hivi, tunapaswa kuwa tofauti na wakorintho waliohukumu kwa mtazamo wa kibinadamu na kuona uzuri wa mtu kwa namna ya kibindamu. Badala yake tumshukuru Mungu ya kwamba anajenga ufalme wake kupita udhaifu, na aibu, na unyonge, na upuzi (1 Kor 1:18-25). Hata katika sisi nguvu zake zinaonekana kwa udhaifu wetu.

Tatu, Paulo alijisifia udhaifu na mateso na adha na vingine ambavyo ni kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya watu kusikia Injili (taz. 2 Kor 4:7-12) na kwa sababu Mungu hutumia kwa utukufu wake. Yesu alisulubiwa kwa udhaifu na aibu, akafufuliwa kwa utukufu na nguvu. Kwa sisi, utukufu ni kwa ufufuo wetu baadaye, na kwa sasa ni udhaifu na aibu, ni njia ya msalaba, na katika hivi Mungu ataonyesha udhaifu wake.

Neema yangu yakutosha! Bwana Asifiwe!

Neno la Siku 1: Efe 3:10-11

ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu.


Hapa Paulo aliongea jambo la ajabu la kwamba Mungu amewapatanisha watu — wapatane na Mungu kwa kusamehewe dhambi zao kwa neema (2:1-10) na pia wapatane wao kwa wao na hasa Wayahudi na wa Mataifa kwa kuondoa kizuizi chao (sheria).

Hili ni jambo la kushangaa na kumsifu Mungu. Lakini tukisoma mistari hii tutashangaa zaidi kwa sababu inaeleza kuwa Mungu alipanga tangu awali kuonyesha hekima yake kwa njia fulani. Njia hii ni huo upatanisho na hekima yake Mungu inaonekana katika upatanisho huo — wenye dhambi waliosamehewa kwa neema kukusanyika pamoja.

Bali sijui kama uliona — hekima hiyo inaonekana lini na wapi? Ni sasa — yaani katika siku hizi baada ya kupaa kwake Yesu na kabla ya kurudi kwake. Na ni katika kanisa ambapo Mungu anaonyesha hekima yake. Hapa kwa neno kanisa Paulo anamaanisha watu wanaokusanyika kwa pamoja mahali fulani — ikiwa Moivaro, Dereda au Muleba.

Ala! Kanisa lako dogo (au kubwa) ni uthibitisho wa hekima ya Mungu. Si jengo, bali watu wale waaminio. Mungu anaonyesha hekima yake kwa malaika na vyote vya kiroho kwa kuwaonyesha kanisa lako — wapate kuona watu walio wafu kwa sababu ya dhambi wenye uhai kwa neema, na kukusanyika pamoja katika Roho Mtakatifu na upendo.

Ebu tafakari maneno yake Paulo hapa. Ni jambo zuri sana. Na fikiri hivi mara ijayo ambapo utakusanyika pamoja na waumini wa kanisa lako: falme na mamlaka za mbinguni wanawatazama — wakiona paa ya kanisa lako limeharibika, na kwamba hujapata madirisha bado, na kuona yaliyomo kikapuni si mengi, na kwaya huimba bila vyombo, bali wanaona nini? Wanatazama hekima ya Mungu na kusudi lake la milele na kumsifu Mungu jinsi alivyo mkuu kwa sababu wanaona ukweli — wafu kuishi, wenye dhambi kusafishwa na walio na uadui kupatanishwa!

Bwana Yesu Asifiwe!